
Mnapaswa kufanya kikao cha kuandaa IFSP mapema iwezekanavyo ila isizidi siku 45 tangu mtoto wako kupewa rufaa kwenda programu ya EI. Hakuna tozo wala gharama za kuandaa mpango. Mratibu wako wa huduma na timu yako ya EI watakusaidia:
- kutambua wasiwasi na vipaumbele vya kukidhi mahitaji ya mtoto wako,
- kuandaa matokeo ya IFSP kwa ajili ya mtoto wako na familia yako,
- kukubali huduma na usaidizi ili kumsaidia mtoto wako na familia yako kukidhi matokeo hayo yaliyotambuliwa, na
- kuamua iwapo huduma zinalipiwa ada.
IFSP ni Nini?
IFSP ni mpango ambao unauandaa pamoja na timu yako ya EI. Mpango huu unaakisi vipaumbele na wasiwasi wako kwa mtoto wako. Wewe ndiye unayebaini matokeo (k.m., mtoto wako kutembea, mtoto wako kutamka neno, mtoto wako kuwa wa kwanza kukumbatia) ambayo unayataka kwa mtoto na familia au walezi wako. Hizi ni kauli ambazo zinaelezea mabadiliko na faida ambazo unataka kuziona kwa mtoto wako na familia yako. Wewe na timu yako pia mtabaini huduma za kufikia matokeo haya.
Unaweza kuanza kwa kuuliza maswali mawili:
- Faida gani nataka mtoto na familia yangu izipate kutoka EI?
- Nini kitakuwa tofauti au bora kwa mtoto wangu na familia yangu wakati mabadiliko haya yatakapofanyika?
Huduma zilizoainishwa katika IFSP zinakusudia kuunga mkono matokeo makuu matatu:
- Kupata na kutumia maarifa na ujuzi.
- Kujenga mahusiano chanya ya kijamii.
- Kutumia tabia sahihi kukidhi mahitaji yake.
Itajumuisha pia matokeo ya familia. Matokeo matatu muhimu (tazama Nyongeza F) yanajumuisha:
- Kuelewa nguvu, uwezo na mahitaji ya mtoto wako;
- Kumsaidia mtoto wako kukua na kujifunza; na
- Kujua haki zako za kisheria kuhusiana na huduma za mtoto wako.
Nani Anapaswa Kuhusishwa katika Kuandaa IFSP?
Mratibu wako wa huduma atakuelezea mchakato wa IFSP na kupanga kikao cha kuweka mipango ya IFSP. Mratibu wa huduma atashirikiana nawe kupanga tarehe na eneo ambalo linafaa kwako. Utapata notisi ya maandishi inayothibitisha kikao husika. Kikao kinapaswa kuendeshwa kwa lugha yako ya asili. Unaweza kuomba mkalimani ikiwa unazungumza lugha tofauti na Kiingereza na utapewa mmoja, ikiwa atapatikana.
Kikao kitajumuisha wewe, mratibu wa huduma, na timu ya kufanya tathmini. Unaweza kualika familia, marafiki, au mtu yeyote atakayehusika. Kumbuka kwamba wewe ni mshirika mwenye haki sawa katika kupanga na kuunda mpango huu.
Kwa Nini IFSP Inatakiwa Kusainiwa?
Mara baada ya wewe na timu yako kukubaliana matokeo na huduma za IFSP, utasaini na kupewa nakala ya mpango. Saini yako inaonesha umeukubali mpango kama ulivyoandikwa, au mabadiliko uliyoainisha katika ukurasa wa utekelezaji. Mratibu wako wa huduma pia atakusaidia kubaini iwapo utahitajika kulipa ada ya kila mwezi ya ushiriki wa familia katika huduma za EI kulingana na kipato cha familia yako na mambo mengine.
Wewe na timu yako ya IFSP mtapitia maendeleo ya mtoto kila baada ya miezi sita na kuboresha mpango angalau mara moja kwa mwaka. Mahitaji yako yakibadilika, wewe na timu yako mnaweza kukutana mara nyingi zaidi ili kuubadili mpango kadri itakavyohitajika.
Hatua Inayofuata: Huduma za msaada wa mapema

